BARAZA LA WAFANYA KAZI LAZINDULIWA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SIMIYU
Posted on: September 19th, 2020Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu tarehe 19 Septemba, 2020 imezindua Baraza lake jipya la Wafanyakazi, ambapo Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo alikuwa ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu , Bi Miriam Mmbaga.
Aidha kabla ya uzinduzi huo Bi Miriam alianza kwa kutembelea sehemu mbalimbali za kutolea huduma zikiwemo Wodi, Maabara, Famasi, Chumba cha Mionzi na Upasuaji Mkubwa pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto
Picha: Bi Miriam Mmbaga akikagua ujenzi wa Jengo la Afya ya Mama na Mtoto unaoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu
Uzinduzi huu uliambatana na kufanyika kwa uchaguzi wa Katibu Mpya, ambapo Dkt Patricia Robert Mbwasi alishinda kwa kura kumi na tatu dhidi ya kura nane alizozipata mpinzani wake Ndugu Ibrahim Wilubulambu, na kumfanya Dr Patricia kupitishwa kuwa Katibu wa Baraza la WafanyaKazi, Hata hivyo Ibrahim Wilubulambu alifanikiwa kuwa Katibu Msaidizi wa Baraza hili jipya. Aidha, Mganga Mfawidhi wa Hospitali Dr Matoke Muyenjwa ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Mkoa wa Simiyu.
Kwa upande mwingine wajumbe walipiga kura za kumchagua Mwakilishi wa Baraza Kuu la Wafanyakazi Wizarani ambapo Ndugu Saimon Sospeter aliibuka kuwa mshindi kwa kupata kura tisa dhidi ya wapinzani wake, Ndugu Mugisha Kahigi ambaye alipata kura saba na Dkt Hierecenter Silyimbo ambaye alipata kura sita. Na hivyo wajumbe waliridhia kuwa Ndugu Saimon Sospeter atakuwa mwakilishi wa Baraza la Wafanyakazi wa Hospitali katika Baraza Kuu la Wafanyakazi. Aidha Afisa kazi Kanda ya Ziwa Ndugu Goodluck Luginga ambaye alieleza kuwa uawakilishi huo wa Ndugu Saimon wa kipindi cha miaka mitatu ambao unaweza kukoma endapo ataachishwa kazi, kuhama au kutohudhuria vikao vitatu bila kutoa taarifa kwa mwenyekiti.
Picha: Ndugu Saimon Sospeter akitoa shukrani baada ya kupata nafasi ya kuchaguliwa kuwa mwakilishi katika Baraza kuu la Wafanyakazi.
Baada ya Hayo, Mgeni Rasmi, Bi Miriam Mmbaga alishukuru uongozi wa Hospitali kwa kuanzisha baraza la Wafanyakazi ambalo alisema litakuwa ni chombo cha kuongeza ufanisi, kupunguza malalamiko na kero ndani na nje ya taasisi na kuongeza morali ya kazi kwa watumishi wote.
“Baraza liwe ni sehemu ya kupokea mawazo, hoja za wafanyakzi ikiwa ni sambamba na kuweka mifumo mizuri ya kupokea maoni, ushauri na malalamiko ya wateja mnaowahudumia. Pia natoa pongezi kwa idara ya Maabara kwa kupata nyota tatu katika mchakato wa kupata ithibati na kwamba kila mtumishi anatakiwa atende kazi kwa kuzingatia Dira ya Hospitali ili kuongeza ushindani wa utoaji huduma katika mkoa na Tanzania kwa ujumla” Alisema Bi Mirium.
Vilevile Bi Mirium aliipongeza Hospitali kwa kazi nzuri iliyofanyika katika maonyesho ya nanenane
Picha:Mgeni Rasmi (Bi Miriam Mmbaga) akitoa neno kwa Wajumbe wa Baraza jipya la Wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa waSimiyu
Baada ya hayo mgeni rasmi Bi Mirium alilizindua rasmi Baraza la Wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu kwa kukata utepe katika kitabu cha mkataba wa kuunda baraza la wafanyakazi
Picha: Bi Miriam Mmbaga pamoja na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Simiyu wakiwa wameshikilia kitabu cha Mkataba wa Baraza la Wafayakazi baada ya kukata utepe katika kitabu hicho kama ishara ya uzinduzi wa Baraza hilopicha: Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi Bi Catherine (aliyesimama) akitoa mchango katika mada mbalimbali zilizotolewa katika kikao hicho
Aidha Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa, Dkt Kulemba alimshukuru Mgeni Rasmi kwa kuzindua baraza na kuwataka wajumbe wa baraza kuwa mfano mzuri wa kuigwa na chombo cha kuondoa migogoro kazini. Aliwashukuru viongozi wa hospitali hususani Afisa Utumishi Mkuu I Ndugu Protace Magayana na Mganga Mfawidhi wa Hospitali Dkt Matoke Muyenjwa kwa kazi nzuri wanazofanya ili kuimarisha utoaji wa Huduma.
Baada ya ufunguzi huo wajumbe wa Baraza la wafanya kazi walipitishwa katika mada mbalimbali zianazohusu shughuli zao
Picha: Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakifuatilia Mada inayohusu Majukumu yao iliyotolewa na Afisa Kazi wa Kanda ya ziwa Ndugu Goodluck Luginga
Picha: Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakiwa katika Picha ya pamoja na Mgeni Rasmi Bi Miriam Mmbaga