Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu
(Simiyurrh)

SAMIA AZITOA WASIWASI NCHI WANACHAMA WA SADC JUU YA UWEZO WA MSD.

Posted on: November 9th, 2019

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluh Hassan amezitoa wasisi Nchi wanachama wa SADC kuwa Bohari kuu ya Dawa (MSD) imejipanga vizuri kuhakikisha jukumu la uratibu wa manunuzi ya pamoja linatekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu.

Ameyasema hayo leo wakati akifungua Mkutano wa pamoja wa Mawaziri wanaosimamia Sekta ya Afya na UKIMWI wa Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), katika ukumbi wa BOT, Jijini Dar es salaam.

“Nitumie fursa hii kuwahamasisha nchi wananchama wa SADC kuwa MSD imejipanga vizuri kuhakikisha jukumu hili la uratibu wa manunuzi ya pamoja unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa” Amesema Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande mwingine, Mhe. Samia alisema katika kipindi cha miaka mine, vituo vipya vya afya 352 vimejengwa na maeneo mbalimbali, ngazi ya kata, hospitali 67 katika ngazi ya Wilaya na hospitali 6 za mikoa katika kurahisisha utoaji huduma za afya.

Mbali na hayo, Mhe. Samia alisema Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya dawa kutoka vyanzo vya ndani kutoka Sh30 bilioni kwa mwaka 2015/2016 hadi kufikia Sh260 bilioni 2019/2020, ikiwa ni juhudi za Serikali katika kuwahudumia Wananchi wa hali zote katika jamii.

“Vilevile Serikali kupitia Taasisi yake ya MSD imetengeneza mfumo wa ugavi unaosimamia manunuzi ya pamoja ya dawa na vitendanishi kwa lengo la kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za manunuzi nchini na kwa nchi wanachama wa Sadc, hii yote ni katika kufikia afya kwa wote,” alisema.

Aidha, Mhe. Samia alisema, tayari Tanzania iliashaanza kuandaa mazingira ya kuingia katika mchakato huo kwa kuwekeza katika sekta ya afya na kuweka mifumo madhubuti inayowawezesha wananchi kumudu gharama za matibabu.

“Ili kufikia lengo la afya bora kwa wote na kutatua changamoto ya ugharamiaji wa huduma za afya, Serikali inatarajia kuanzisha bima ya afya kwa wananchi wote, hali itayosaidia Wananchi kumudu gharama kubwa za matibabu”, alisema.

Mhe. Samia aliendelea kusema kuwa, Kwenye suala la kufikia lengo la afya kwa wote, Serikali ya Tanzania imeweka kipaumbele katika kuimarisha miundombinu na mifumo ya afya hususasn katika kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa kwa kuzingatia ubora.

Nae, Meneja wa kanda ya Afrika kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Rebeca Matshidiso Moeti alisema kuwa, ni muhimu kila mwananchi kupata huduma za afya bila vikwazo kiuchumi, hii itaongeza thamani ya maisha.

“Mpango wa huduma ya afya kwa wote umeweza kusaidia kuokoa maisha pamoja na kuongeza thamani ya maisha kwa wananchi wengi, hasa katika nchi ambazo zimeshaanza utekelezaji,” alisema Dkt. Rebeca Matshidiso Moeti.

Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa, “Jumuiya ya SADC ilisaini itifaki ya afya (protocol health) mwaka 1999 ambayo ilizinduliwa mwaka 2004 kwa ajili ya kutoa muongozo wa masuala ya afya na UKIMWI, ,jumuiya ilianzisha mkakati wa maendeleo wa kanda kwa kipindi cha miaka mitano.
Aliendelea kusema kuwa, Mawaziri wa SADC wanaoshughulika na masuala ya UKIMWI wamekua wakikutana kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa program mbalimbali za afya na UKIMWI zilizoainishwa katika kipengele B cha mkakati huo.

“Mawaziri wenzangu leo tuna wajibu mkubwa wa kupitia, kujadili na kuridhia mapendekezo yatakayowasilishwa na wataalamu ambayo yanalenga kuhakikisha utekelezaji wa maazimio hayo pamoja na kulinda maslahi ya jumuiya yetu”, alisisitiza Waziri Ummy.


Chanzo wizara ya afya