HOMA YA INI
Posted on: November 3rd, 2019Ini ni kiungo muhimu sana ndani ya miili yetu, hufanya kazi zaidi ya 500 ; moja ya kazi ni kuchuja na kuondoa sumu kutoka kwenye damu.
Kutokana na sababu mbalimbali kama pombe iliyopita kiasi, sumu kwenye damu au maambukizi; ini hupata shida na kuvimba na kushindwa kufanya kazi vizuri. Hii hali huitwa HOMA YA INI au HEPATITIS.
Katika maeneo yetu, bara la Afrika maambukizi ya virusi wa Homa ya ini ndio sababu kuu ya shida kwenye ini. Virusi vya Homa ya ini vipo vya aina 5 (A,B,C,D,E).
Aina mbili za virusi (B na C ) ndio sababu kuu za ugonjwa wa homa ya ini na husambaa kupitia damu na majimaji ya mwili.
Homa ya ini ni sawa janga linaloua kimya kimya kulingana na takwimu za vifo za dunia inakadiriwa Kirusi cha homa ya ini aina ya B pekee huua watu 600,000 hivi kila mwaka.
Kwa wastani zaidi ya watu bilioni mbili, yaani, asilimia 33 hivi ya watu wote ulimwenguni, wameambukizwa virusi vya HBV, na wengi wao hupona baada ya miezi michache. Watu milioni 350 hivi huendelea kuwa na virusi hivyo mwilini, wengi huishi bila dalili na kuendelea kuambukiza watu wengine
JINSI UNAVYOAMBUKIZWA:
Katika maeneo hatari zaidi duniani, Virusi vya Hepatitis B (HBV) kwa kawaida husambazwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kuzaliwa au kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine hususan nyakati za utotoni.
Kama ilivyo kwa Ukimwi, Virusi vya Homa ya Ini pia huambukizwa kwa njia ya kujamiiana, mate, jasho na mwingiliano wowote ule wa damu.
NJIA KUU ZA MAAMBUKIZI
|
---|
Kuchangia miswaki. |
Kujamiana bila kinga. |
Kunyonyana ndimi 'denda'. |
Mama mwenye ugonjwa kumwambukiza mtoto wakati wa kujifungua. |
Kuchangia damu isiyo salama.
|
Kuchangia vitu vya ncha kali kama sindano, wembe n.k |
kuchangia taulo na mwenye ugonjwa huo. |
kubadilishana nguo au kukumbatiana wakati mkiwa mnavuja jasho. |
Tafiti za kitaalamu zinaonesha kuwa virusi hivyo ni hatari kuliko hata vya Ukimwi kwa sababu vinaweza kuishi nje ya mwili wa binadamu (yaani nje ya mfumo wa damu) kwa siku saba. Virusi vya Ukimwi (VVU) havina uwezo wa kuishi nje ya mfumo wa damu hata kwa dakika moja.
Kutokana na usugu wa HBV, maana yake ni kwamba kama kirusi kipo kwenye ngozi, kitaendelea kuwa hai kwa siku saba na katika kipindi hicho mtu anaweza kuambukizwa kwa njia ya damu au jasho.
Kwa wastani kirusi cha HBV kikishaingia mwilini, hupevuka ndani ya siku 75, hata hivyo upo uwezekano wa kupevuka kati ya siku 30 hadi 180. Ndani ya siku 30 mpaka 60, mtu mwenye HBV anaweza kugundulika ikiwa atapimwa.
Mtu mwenye Homa ya Ini ana wastani mdogo wa kuishi kuliko mwenye Ukimwi. Kwa maana hiyo, mwenye maambukizi ya Virusi vya Homa ya Ini hufariki dunia haraka kuliko mwenye VVU.
DALILI ZA UGONJWA HUU:
Watu wengi hawaonyeshi dalili yoyote. Kwa maana hiyo mtu anaweza kuishi na HBV na kusababisha maambukizi kwa wengine bila kugundulika.
Hata hivyo, watu wengine husumbuliwa na homa kali na dalili ambazo hudumu kwa wiki kadhaa.
DALILI
|
---|
Uchovu |
Kichefuchefu |
Mwili kuwa Dhaifu |
Homa Kali |
Kupoteza hamu ya kula |
Kupungua Uzito |
Maumivu makali ya tumbo upande wa ini |
Macho na ngozi kuwa vya njano |
Mkojo Mweusi |
UJUMBE
Pata chanjo ya homa ya ini ili kuweza kujikinga na ugonjwa huu.