Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu
(Simiyurrh)

KATIBU MKUU AFYA ATEMBELEA SIMIYU

Posted on: October 22nd, 2019

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula ameendelea na ziara yake ya Mikoa ya kanda ya ziwa kwa kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu ili kuona hali ya miundombinu na utoaji wa huduma za afya.

Dkt. Chaula ameridhishwa na ujenzi wa Hospitali hiyo ambao umekamilika kwa asilimia zaidi ya 98 na kinachosubiriwa ni ufungaji wa vifaa vya Radiolojia na upasuaji ili huduma hizo zianze kutolewa haraka iwezekanavyo huku huduma wa wagonjwa wa nje (OPD) zikiwa zimeshaanza.

Kwa mujibu wa Injinia Mkuu wa Wizara ya Afya Francis Mbuya amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa mkandarasi wa Hospitali hiyo Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) atamalizia maeneo machache yaliyobaki ikiwemo ufungwaji wa mabenchi ya maabara na kukabidhi jengo ifikapo Mwezi Disemba mwaka huu.

Kabla ya kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Katibu Mkuu Dkt. Chaula alitembelea Hospitali ya Wilaya na kisha kuongea na watumishi ikiwa ni pamoja na kuwasikiliza kero zao, kuzitatua na kuwataka kuwatumikia wananchi kwa moyo mmoja.