Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu
(Simiyurrh)

WAZIRI MKUU AWAASA WANANCHI KUJENGA UTAMADUNI WAKUFANYA MAZOEZI.

Posted on: November 16th, 2019

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa amewaasa Wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi walau mara tatu kila wiki kwa dakika 30.

Ameyasema hayo leo, wakati akizindua Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyo yakuambukiza katika viwanja vya Jamhuri, Jijini Dodoma.

Mbali na hayo, Waziri Mkuu, amesisitiza juu ya kupunguza matumizi ya vilevi, kama vile Pombe na sigara pamoja na kinywaji vyenye sukari, ambavyo kwa kiasi kikubwa huchangia magonjwa kama vile kisukari na Kansa jambo linalopelekea mzigo wa matibabu kwa wananchi.
Ameendelea kusisitiza kwa kuwaagiza viongozi wa maeneo mbali mbali kuhamasisha wananchi wa maeneo yao kufanya mazoezi angalau kila juma mosi, na kuwataka kupunguza matumizi ya magari kila mara.

Aidha, Mhe. Majaliwa ameagiza viongozi kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi vya kufanya mazoezi, na kusisitiza kuvifufua vikundi vyote vya mazoezi vilivyo kufa, huku akieleza umuhimu wa kutoa taarifa kwa wananchi ili washiriki katika mazoezi.

Amesema Halmashauri zote zihakikishe zinatenga na kuyaendeleza maeneo ya wazi katika kila kata au mitaa ili pamoja na shughuli nyingine wananchi pia watumie maeneo hayo kwa ajili ya kufanya mazoezi.

Waziri Mkuu amewataka wanafunzi kuanzia sasa kabla ya kuingia darasani wawe wanakimbia mchaka mchaka ili waweze kujiimarisha kiafya jambo ambalo litawaepusha na magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalim amesema kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Tanzania ilishuhudia ongezeko la idadi ya watu waliopatiwa huduma za magonjwa yasiyoambukiza kutoka wagonjwa milioni 3.4 kwaka 2016 hadi wagonjwa milioni 4.2 mwaka 2018, ilkiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 24.

Hata hivyo, Waziri Ummy ameyataja magonjwa hayo ni kama vile, pumu, shinikizo la juu la damu, kisukari, saratani, siko seli, magonjwa ya akili, ajali, magonjwa mengi ya macho, kinywa, masikio, pua na koo, huku akidai kuwa magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka duniani kote na kuathiri nyanja zote za kimaisha